Tumshukuru mwenyezi Mungu kwa
kutufikisha mwaka 2016 salama na wale ambao wametangulia mbele za haki mungu
awapumzishe salama.
Nimeamua kuandika makala hii
baada ya kutoka safarini wilayani RUNGWE. Wakati wa matembezi yangu niliona
mmea ninaoufahamu umepandwa kwa mzee mmoja wa kinyakyusa.
Nikakumbuka kuwa hata mimi
nimepanda nyumbani kwangu Mbeya. Ikabidi nimwone huyo mzee ili niweze kupata
maelezo ya mmea huo na akanikaribisha.
Nikajitambulisha mimi ni nani na
natoka wapi. Na yeye akajitambulisha yeye ni nani. Ndipo nilipomweleza shida
yangu iliyonipeleka kwake. Yule mzee aliniambia kuwa ule mmea ameurithi kutoka
Kwa baba yake mzazi. Akanieleza kuwa miaka zaidi ya 50 njaa iliwahi kutokea
unyakyusani na viazi hivyo viliwaokoa wakati wa njaa. Na akaniambia kwamba mzee
wake alisema kamwe asiupoteze maishani mwake. Mmea huu kwa kibotania huitwa
Dioscorea bulbifera. Waingereza huita Air potato au Bitter yam, Wanyakyusa
huita ngengele. Na husitawi kwa mtindo wa kutambaa kwenye miti kama chayote au
pesheni.
Na inaweza kukua inchi 8 kwa siku
na wastani kufikia futi 60.Na huweza kufika futi 150 kwa urefu kufuatana na
eneo lilivyo rafiki na mmea wenyewe. kuna aina zingine ni chungu na haziliwi.
Dioscorea bulbifera na Dioscorea Deltoidea ndio huliwa. Lengo langu kubwa ni
kwa watanzania kuanza kufufua mazao yaliyokuwa yakilimwa na mababu zetu na
kutumiwa kwa chakula lakini yameachwa kwa sababu ya kwenda na wakati.
Huko Kenya kabila la Tiriki wanaita
marugu (Dioscorea bulbifera) wanasema ni chakula bora kuliko mkate wa ngano
mweupe.Wanasema wakila marugu hukaa muda mrefu tumboni bila kusikia njaa. Hapa Tanzania
tunatakiwa tuendeleze zao hili na yale mengine ambayo hayatiliwi maanani.
Dioscorea bulbifera ina
flavonoids na isoflavonoids vitu ambavyo ni muhimu kwa afya zetu.
Ngengele huzuia/ hutibu kuharisha,
kuhara damu, Homa ya manjano, maumivu ya tumbo, Anorexia, conjunctivitis, na
mzio unaosababishwa na kuumwa na wadudu kama spider na whip spider. Wenzetu
wahindi na wachina hutumia kutibu maumivu ya koo, saratani ya tumbo na goita.
Wapangwa wa Ludewa huita Ing’ing’i hutumia kuondoa matego kwa watu waliofanyiwa
hivyo. Wanyakyusa hula baada ya kuvichemsha au kuviweka kwenye majivu ya moto
mpaka vikaiva. Aina ya Dioscorea deltoidea huliwa na wale wanaotaka kuwa
mabaunsa (body-builders) na wale wanaotaka kuongeza Testosterone mwilini.
ANGALIZO
Kuna aina nyingi za Ngengele
zingine ni chungu unapokula, kwa hiyo hakikisha unatumia zile ambazo zinafaa
kuliwa. Ngengele haziko kundi moja na viazi vitamu.
No comments:
Post a Comment